MHESHIMIWA Rais wangu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Nakusalimu kwa salamu
ya utii inayotambua na kuheshimu kwa dhati mamlaka makubwa na ya juu
uliyonayo kama mkuu wa taifa letu ambalo mazingira yake ya leo yanapaswa
yawe wenye mwelekeo wa kushangilia kama si kujivunia uhuru ambao
tuliupata mwaka 1961 na 1964 kwa kutegemea upande tulipo katika muungano
wetu.
Mheshimiwa Rais, najisikia faraja iliyojaa majonzi moyoni kupata fursa
hii adhimu kukuandikia waraka ambao msukumo wake unasukwasukwa na
dhamira njema kabisa ambayo aghalabu kiini chake si kingine bali mapenzi
mema kwa nchi na viongozi wetu wote.
Ni faraja kwa kuwa nimepata fursa ghali na adimu ya kuteta na kiongozi
wetu mkuu kwa upendo, uhuru na kwa kujiamini, huku nikiwa na uchungu
pia kwa sababu ujumbe ambao unabebwa na waraka huu ni wa kuumiza sana
nafsi, roho, akili na mwili.
Mheshimiwa Rais, wewe ni kiongozi wa Watanzania wote tukiwamo sisi
ambao baadhi ya wateule wako wameamua kwa sababu wanazozijua wao na
wakati mwingine wakidai kwa maelekezo ya wakuu wao kutujengea taswira
zinazotufanya tuonekane tu watu wa ovyo na kada ya wanajamii waliokosa
utu na eti tunaopaswa kufundishwa hekima na somo la uzalendo ambalo
limekuwa sehemu ya makuzi yetu nyumbani, shuleni, jeshini na ndani ya
jamii.
Kabla sijafikisha ujumbe ambao nimeubeba kwa mfano wa mzigo mzito
moyoni, napenda kwanza kupitia fursa hii kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi
Mungu, mwingi wa rehema na neema kwa kuniwezesha kuuona mwanga wa siku
hii njema ya leo ambayo kama si kwa kudra na mapenzi yake, yumkini
ingeongeza hesabu za siku ambazo kiwiliwili changu kingekuwa katika
kaburi la sahau ambalo kila kukicha linameza roho za makumi kama si
mamia ya Watanzania wasio na hatia wanaopoteza maisha kutokana na kazi
za mikono ya majahili, miungu watu waliojitwalia haki ya kuchagua aina
ya maisha na vifo vya watu wengine.
Baada ya hilo, kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania wenzangu ambao
hawana fursa ya kuwasiliana nawe kwa njia kama hii ya waraka
niliyoitumia, napenda kutumia pia wasaa huu kukushukuru wewe binafsi
kwa namna ulivyojitoa usiku na mchana pasipo kuchoka kuliongoza taifa
hili katika mazingira magumu yaliyojaa changamoto za kila namna ambazo
wakati mwingine sina shaka hata kidogo kwamba zimekuwa zikikunyima raha
na kukosa usingizi.
Wakati nikikuandikia ujumbe huu, picha na taswira yako inayonijia ni
ile ya Machi 8, mwaka huu siku uliponitembelea kando ya kitanda
nilichokuwa nimelazwa katika Hospitali ya Milpark, Johanesburg kule
Afrika Kusini ikiwa ni siku mbili tangu nilipovamiwa, nikajeruhiwa na
kupewa ulemavu na majahili ambao hadi leo hii wameweza kuukwepa mkono
mrefu wa vyombo vya dola unavyoviongoza.
Mheshimiwa Rais, japo nilikuwa nina maumivu makali na machungu ya
kupoteza jicho, kidole na kupasuliwa kwa mifupa ipatayo minane katika
paji langu la uso, ukiacha taya lililoachanishwa kikatili na watesi
wangu wale, bado ninaweza kukumbuka kwa ufasaha namna ulivyozungumza
nami ukionyesha jinsi ulivyokuwa ukiguswa na kuumizwa sana na tukio
lile.
Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, tangu niliporejea nchini miezi
sita iliyopita sijapata kukutana nawe ana kwa ana ingawa nilipata fursa
ya kukutumia salamu zangu za shukrani kupitia kwa marafiki zako kadhaa
akiwamo msaidizi na mshauri wako nambari moja, Makamu wa Rais, Dk.
Mohammed Gharib Bilal ambaye siku zote wakati nikiwa katika matibabu
nchini Afrika Kusini na hata baada ya kurejea nchini, alionekana kuwa
mtu wa kukosa amani kabisa pasipo kunijulia hali kwa njia ama ya simu,
wasaidizi wake na mwisho kwa kuonana nami ana kwa ana.
Nayarejea haya yote huku nikitambua kwamba, wakati ninapoandika waraka
huu ndiyo kwanza umerejea kutoka nchini Marekani ambako ulikwenda
kuchunguzwa afya yako ambayo nina matumaini makubwa ni njema hasa kwa
kuzingatia ukweli kuwa, ulikwenda huko siku chache tu baada ya
kuiwakilisha vyema nchi yetu katika msiba mzito wa shujaa wa mapambano
ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, mzee wetu, Nelson Mandela.
Ninapoyatafakari matibabu ghali niliyopata nchini Afrika Kusini kwa
msaada wa mwajiri wangu na safari yako nchini Marekani, vinanikumbusha
swali la mmoja wa wasaidizi wangu hapa ofisini aliyetaka kujua ni
sababu gani hasa ambazo zimekuwa zikisababisha wasomi na viongozi wetu
kuchunguzwa na kutibiwa katika hospitali za nje, tofauti na ilivyokuwa
kwa Madiba ambaye kwa nyakati zote tangu afya yake ianze kumtatiza
alikuwa akipata matibabu huko huko kwao Afrika Kusini?
Niseme kweli, japo nilikuwa na jibu au majibu ya swali lake, sikuwa na
maelezo ya kutosheleza yaliyokuwa na mwelekeo wa kukata kiu ya swali
lake, ingawa kwa kupapasa nilifanya kila juhudi kuutetea utaifa wangu
na viongozi wake ilhali miye mwenyewe nikiendelea kukosa raha kwa namna
nilivyokuwa nikitoa majibu ambayo yalikuwa yakionyesha hali ya
kuukubali unyonge, kukiri ufukara, kuficha udhaifu wetu kama taifa na
kutetea makosa ambayo aghalab ninyi viongozi wetu na wale wa kabla yenu
mngeweza kuwa watu mliostahili kuwa na majibu halisi.
Rais wangu, swali na majibu vilisababisha kimoyomoyo, nijiulize maswali
mengi mengine na moja ya maswali hayo yakiwa ni wapi tulipopotea njia
hata tukafikia hatua ya kusababisha kuwa na kundi kubwa la watu
waliokata tamaa, wanaoteswa na ufukara, ukosefu wa ajira na kila aina
ya kero na karaha zinazozonga maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Rais, hali hiyo ilinipeleka moja kwa moja nchini Afrika
Kusini na hususan katika Hospitali ya Milpark ambako huko ndiko miye
mwenyewe na Watanzania wenzangu wengine tulikonusuru maisha yetu, huku
baadhi kama ilivyo kwa Dk. Sengondo Mvungi wakipoteza maisha yao baada
ya kukimbizwa huko.
Mheshimiwa Rais, naomba unisamehe kwa kulisema hili nitakaloliandika
hapa kwamba, jibu nililolipata haraka haraka kuwa moja ya chagizo la
matukio ya namna hii kutokea, halikuwa jingine bali ni kushindwa
kuwajibika ipasavyo kwa viongozi wetu hususan wale tuliowapa dhamana ya
kuongoza sekta kadhaa nyeti kama ya afya na ustawi wa jamii.
Ushahidi wa kupwaya huko kwa viongozi hususan wale walio chini yako,
ndiko huko huko ambako kumedhihirika pia wiki iliyopita bungeni Dodoma,
ambako tulishuhudia zahama nyingine iliyowang’oa madarakani mawaziri
wako muhimu wanne kwa sababu kama hizo hizo za mkwamo wao au watendaji
wa chini yao katika kusimamia ipasavyo na kuchukua hatua kwa wakati,
kila yatokeapo matatizo yanayogusa maeneo wanayoyaongoza.
Nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu, mheshimiwa Rais iwapo nitaficha
shauku ya moyo wangu ambayo ilikwenda sambamba na tukio lile la Dodoma
lililowagusa baadhi ya mawaziri ambao anguko lao linaweza likaelezwa
kuwa ni ‘ajali ya kisiasa’ nikitumia msamiati ulioutumia wewe mwenyewe
kwa mara ya kwanza ulipozungumzia tukio la kujiuzulu kwa waziri wako
mkuu wa kwanza, Edward Lowassa.
Haja ya moyo wangu, nikiwa mhariri, mwanahabari, Mwenyekiti wa Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF) na mdadisi wa kawaida tu wa mambo, ilikuwa
kuona anguko la namna hiyo hiyo likimfika Waziri wa Habari ambaye
amethibitisha pasipo na shaka kuwa pamoja na kuwa msomi wa Shahada ya
Falsafa (Phd), ni kiongozi asiyejua anachofanya kwa kiwango cha kuwa
mtu ambaye vichwa vya watu wengine ndivyo vinavyofikiri kwa niaba yake.
Nilitamani afikwe na zahama hiyo si kwa sababu ya kuwa na hasira au
kumchuria mabaya, bali kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye ni mtu ambaye
bado anasongwa na matongotongo ya mfumo wa kibabe wa zama za magazeti
ya Serikali na yale ya chama tawala, ambayo yanalazimika kuandika yale
tu yanayofurahisha nyoyo na akili za watawala.
Mheshimiwa Rais, ingawa natambua na kuheshimu ukweli mchungu kwamba,
suala la nani awe waziri na nani asiwe ni jambo la wewe mwenyewe
kupenda na kuchagua na kwamba ulishasema mapema kabisa mbele yetu
kwamba urais wako hauna ubia, bado naamini pia kwamba, wewe ni mtu
msikivu na mkweli uliye tayari kusikia na kustahimili mambo mengi
machungu unayokabiliana nayo kila siku.
Kwa sababu hiyo, basi napenda kukueleza kwa kuweka kumbukumbu sahihi
ili mbele ya safari kabla na baada ya kumaliza urais wako uje
kuyatafakari na kuukumbuka ushauri huu kwako kwamba, waziri uliyempa
dhamana ya kulea na kuendeleza vyombo vya habari, ni mtu wa kuhofiwa,
jeuri, mwenye kiburi, asiyeshaurika na dikteta asiyekutakia mema wewe
binafsi, vyombo vya habari, serikali yako na taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa rais sijui kama unajua kwamba tangu umteue amefanya kazi na
vyombo vya habari vya umma na hata baada ya sisi kufanya juhudi kubwa
ya kuwa karibu naye kikazi kwa makusudi na kwa ujeuri mkubwa, amekataa
wito na kupuuza maoni na ushauri wetu na kwa namna ya kusikitisha
amesikika akitamba waziwazi kwamba anao uwezo wa kulifungia au
kulifutia usajili gazeti lolote ambalo ataliona linakwenda kinyume cha
maadili ya uandishi wa habari.
Waziri huyu ambaye alitarajiwa kuwa na silika za kuwa mlezi bora
kutokana na jinsia yake na historia yake ya kupata kuwa mwanaharakati
kabla ya kuingia serikalini, ndiye ambaye mamlaka makubwa uliyomtwisha,
ameyageuza na kuwa mwavuli wa kuvisulubisha vyombo vya habari vyenye
uthubutu wa kukosoa serikali na kuandika ukweli mchungu ambao
asingependa kuona ukiripotiwa.
Mheshimiwa Rais, pengine baya zaidi kwa tasnia hii ni kwamba waziri
huyo ana bahati mbaya ya kuwa na mmoja wa wasaidizi na washauri wake
katika sekta yetu ya habari ambaye naye, hulka zake tangu aingie katika
tasnia ya habari amekuwa ni mtu wa kujipendekeza, kupenda makuu,
kuzusha na kutokuwa na mawazo huru. Huyu si mwingine bali Mkurugenzi wa
Idara ya Habari (MAELEZO).
Ni jambo la bahati mbaya kwamba waziri huyu msomi pengine kwa sababu ya
kutojua vyema rekodi na historia ya msaidizi wake huyo, ambaye
japokuwa naye pia ni mteule wako, amejikuta akiwa mhanga wa fikra
pandikizi zinazopenyezwa wizarani chini ya uratibu mahususi unaofanywa
na baadhi ya wateule wako ambao wameshaanza kujipanga kusaka urais
baada ya wewe kustaafu.
Mheshimiwa Rais, nimelazimika kuyasema yote haya baada ya kula kiapo
cha moyoni huku nikirejea mafunzo tuliyokuwa tukikaririshwa utotoni
chini ya imani ya wana TANU, ambayo hata sisi ambao hatukuwa wanachama
wa chama hicho tulilazimika kuikariri kwa kuitamka kila kukicha;
‘Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.’
Rais wangu, gazeti la MTANZANIA limerejea tena mitaani. Japokuwa ni
rahisi kuhesabu miezi, napenda kukueleza kwamba, ilikuwa ni miezi
mitatu michungu sana kwetu kihisia na katika hali halisi.
Nitakuwa mzushi sawa sawa na hao ninaowashangaa leo, iwapo nitasema
kulikuwa hakuna hitilafu au makosa ya kiuandishi ambayo yaliwapa
kisingizio cha mikakati waliyoipanga mapema kabisa, wasaidizi wako hao
kwa kulifungia gazeti letu hili.
Mheshimiwa Rais, nasema haya kwa sababu ni ukweli ulio bayana kabisa
kwamba, habari zilizoandikwa na kutoa mwanya kwa serikali yako
kutuadhibu gazeti hili, hazikulenga kuchochea na wala hazikuchochea
kabisa chuki yoyote dhidi ya yeyote na mamlaka unazoziongoza kwa namna
na kwa njia yoyote ile.
Siyo siri hata kidogo, mkurugenzi aliyetangaza uamuzi huo alifanya
hivyo akijua watu wengi hawajui mapito na dhamira yake. Tunajua yeye
alimshauri vibaya waziri na serikali huku akijua vyema kwamba, yuko
hapo alipo kwa maelekezo mahususi ya kundi la watu wenye malengo
binafsi ambao mheshimiwa rais, niko tayari wakati wowote na mahali
popote kukueleza kwa kina na kwa undani ili wakati utakapotaka kuchukua
maamuzi ya haki na kweli ujue undani halisi wa mambo haya.
Leo hii wakati tukirejea tena sokoni, tayari tumeshasikia kuendelea
kuwapo kwa mikakati ile ile ya kuhakikisha gazeti hili na jingine
ambalo halipendwi na watu hao hao kwa sababu binafsi yakiinaingizwa
tena mtegoni na kufungiwa kifungo kingine kama hiki tulichomaliza au
kinachofanana na kile kilichoifika MwanaHalisi.
Mheshimiwa Rais, naandika waraka huu nikikumbuka semi zako mbili
unazotumia; ‘tunajenga nyumba moja kwanini tugombee fito?’ na ile ya
‘akili za kuambiwa changanya na zako’ ambazo kwa muktadha wa waraka
wangu huu kwako zinaweza zikawa za msaada sana kwako na pengine kwetu
sisi wa MTANZANIA ambao tunashangilia kurejea mtaani kwa gazeti letu
lililodhulumiwa fursa ya kuchapwa kwa muda wa siku 90.
Nimelazimika kukutumia wewe Rais si kwa lengo la kuchosha akili zako au
kukupotezea muda, isipokuwa kwa kutambua hadhi, heshima na mamlaka
makubwa uliyonayo juu ya wateule wako hao ambao wameamua kwa sababu ya
jeuri za kimamlaka walizonazo kuumiza watu na kutupa sifa na majina
mabaya tusiyostahili. Hakika wazungu walikuwa sahihi waliposema ‘power
currupts’.
Mheshimiwa Rais, lingekuwa ni jambo la kheri kwa Serikali na kwa taifa
letu zima iwapo kusudi la kufungia magazeti linalopangwa na wateule
wako kuwa utamaduni wa kudumu, lingekuwa ni kujenga mustakabali mwema
kwako wewe binafsi, chama chako, Serikali unayoiongoza na nchi yetu
kuliko hili la sasa lenye dhamira ya kufunga watu midomo, kutesa,
kuzusha na kuharibu taswira yetu kama watu binafsi, taasisi na taifa.
Ni kwa sababu hizo, mheshimiwa Rais ndiyo maana baada ya kusukwasukwa
na moyo na kuumizwa mno kifikra nikaona nitakuwa sijaitendea haki nafsi
yangu na haki za maelfu ya Watanzania ambao tunaamini wanahitaji
huduma ya magazeti haya katika kukidhi mahitaji yao muhimu ya kimaisha,
kielimu na kiufahamu kila kukicha na kuacha dhamira hizi za kishetani
zikiendelea kuongoza sekta yetu.
Mheshimiwa Rais, siyo siri hata kidogo kwamba, ingawa mawazo hasi dhidi
ya uhuru wa kikazi na kiwajibikaji wa vyombo vya habari na wanahabari
yanaonekana kutawala kauli na maamuzi ya baadhi ya viongozi na washauri
wako kwa kiwango cha kukushawishi hata wewe binafsi kukubaliana nayo,
ukweli ni kwamba, nyuma ya maneno matamu wanayotumia kutupaka matope,
kutujeruhi na kutupa kila aina ya sifa mbaya kuna ajenda za kutuharibia
sisi, kukuharibia wewe, kukomoa, kuumiza na zaidi kulikwamisha taifa.
Nitakuwa mhariri nisiyewajibika, iwapo nitakaa kimya ilhali nikijua
fika kwamba, leo hii ndani ya wizara iliyopewa dhamana ya kulea vyombo
vya habari, baadhi ya wateule wako na watendaji wake wamekalia viti
walivyonavyo si kwa sababu ya kuwa kwao na uwezo kustahimili ukosoaji,
au upeo wao wa kuchochea maendeleo ya kitaaluma, bali kwa kuendeleza na
kuyatumikia matakwa ya utarishi wa kifikra na kimatendo.
Kwa waraka huu mheshimiwa Rais, wakati tukikuahidi kwa dhati kabisa
wewe binafsi na Watanzania wenzetu kwamba, tutaendelea na kazi kwa
kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa habari, sambamba na
kuheshimu sheria zilizopo, tunapenda kuliweka hili bayana kwamba,
tutakuwa wa mwisho kuwatii viongozi dhalimu, madikteta, waliokosa utu
na ambao kwao hila ndiyo msingi mama wa kupotosha na kupindisha mambo
kwa sababu tu ya kulinda maslahi na malengo yao binafsi au yale ya
makundi yenye hila.
Rais wangu, nimeona nitakuwa mtu nisiyekutakia mema wewe binafsi na
taifa kwa ujumla, iwapo nitakaa kimya na kuruhusu fikra za kikaburu
zikijijenga vichwani mwa viongozi wetu.
Mheshimiwa Rais, tutakuwa tumeshindwa kutimiza wajibu wetu kama
wanahabari, wahariri na viongozi iwapo tutahalalisha kwa sababu ya
ukimya wetu majina mabaya tunayoitwa leo na wateule wako kama wasaliti,
wachochezi na wazushi.
Miye binafsi naamini kwa dhati kabisa kwamba iwapo wewe utaamua kwa
moyo na nia njema kulinusuru taifa letu na majahili hao walio ndani ya
Serikali yako, basi siku moja historia itakuja kuandika kwa usahihi na
ufasaha jina lako na letu..
Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment