Mbunge wa CHADEMA anusurika kukatwa mapanga

Polisi wakwepa kukamata diwani wa CCM MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, amenusurika kucharangwa mapanga, baada ya kundi la vijana wanaoaminika kuwa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumvamia baada ya kukerwa na hatua ya kuhama kwa karibu uongozi mzima wa chama hicho Kata ya Nduli. Kundi hilo lilimvamia Msigwa alipokuwa akijiandaa kuondoka akiwa na viongozi wanane waliokuwa wa CCM wa kata hiyo, ambao walihamia CHADEMA jana, ambapo walianza kuwashambulia watu walioandamana naye na kuwajeruhi vibaya kwa mapanga watu wawili, kiasi cha kulazimika kukimbizwa hospitalini kwa matibabu. Polisi ambao walipigiwa simu mara baada kuanza kwa vurugu hizo, hawakuweza kujitokeza, hali iliyozusha taharuki kubwa kutoka kwa wananchi waliolazimika kukimbia ovyo ili kuokoa maisha yao. Vijana wanaodaiwa kuumizwa vibaya zaidi ni Oscar Sanga na Seleman Komba, ambao walikuwa miongoni mwa wananchi waliohudhuria mkutano huo. Taarifa za awali zimedai kuwa kundi hilo la vijana lilitumwa na mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa chama hicho, kwa madai ya kukasirishwa na hatua ya kuhama kwa mwenyekiti, katibu na wajumbe sita wa CCM Kata ya Nduli, ambao waliwaongoza zaidi ya wanachama 90 kukihama chama hicho na kujiunga na CHADEMA. Mchungaji Msigwa ambaye aliandamana na Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi (CHADEMA), alifanya mkutano huo akilenga kuwataka wananchi wawe jasiri wa kutambua haki zao na kudai maelezo sahihi ya matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo inayotolewa na serikali katika ngazi za kata na vijiji. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, hakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia vurugu hizo, lakini mmoja wa maofisa wa jeshi hilo alidai hawana taarifa na kwamba watazifuatilia kwa makini kujua kilichotokea na kuahidi kuchukua hatua za kisheria kwa waliohusika na vurugu hizo. Wakizungumza mara baada ya kujiunga na CHADEMA, aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Ayub Mwenda na katibu wake, Godwin Sanga, walisema kuwa wao na viongozi wameamua kukihama chama hicho, baada ya kugundua kuwa kimejaa viongozi wasiokuwa wakweli na wasiojali maendeleo ya wananchi waliowapigia kura. Mwenda pamoja na aliyekuwa mjumbe wa kata hiyo, Temina Ndete, walidai kuwa kwa muda mrefu wamejitahidi sana kupigania haki za wanyonge, lakini hawakuweza kufua dafu kwa sababu uongozi wa juu wa CCM umewatupa na kujali masilahi ya wachache.

No comments:

Post a Comment