Uteuzi wa Mbatia wamkimbiza kigogo
Wakati huo huo, wimbi la wanachama wa vyama vya siasa kutimkia CHADEMA linazidi kushika kasi baada ya aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Buyungu (NCCR-Mageuzi), mkoani Kigoma, Mawazo Metusela, kujivua uanachama.
Metusela (28), alitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam, akidai kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kujiondoa kwenye chama hicho ni kutokana na hatua ya Mwenyekiti wao, James Mbatia, hivi karibuni kukubali uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete wa kuwa mbunge.
Alisema kuwa alithibitisha tuhuma za muda mrefu kuwa NCCR-Mageuzi ni tawi la CCM baada ya uteuzi huo wa Mbatia kuonekana kushangiliwa na kuungwa mkono na viongozi wenzake.
Katika uchaguzi mkuu wa 2010, Metusela alikabana koo na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Injinia Christopher Chiza, akiwa amejizolea kura 11,514 dhidi ya 17,040 za mpinzani wake.
“Mimi wakati huo nilikuwa mwanafunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kimsingi nilishinda uchaguzi huo, ila sema Tume ya Uchaguzi ilinipora ushindi wangu na wananchi walinitaka nifungue kesi kupinga matokeo,” alisema.
Alisema kuwa alipokwenda kuomba msaada kwenye chama wa kufungua kesi, Mbatia alimshawishi aachane na uamuzi huo, akidai Chiza alikuwa ni naibu waziri pekee kutoka mkoani Kigoma, hivyo amwache aendelee na majukumu yake.
Metusela aliongeza kuwa wananchi wa Buyungu walijitahidi kumchangia fedha afungue kesi hiyo, lakini fedha hazikutosha, hivyo baada ya siku 14 Mahakama Kuu Kanda ya Tabora iliifuta.
“Kwa mazingira hayo, wananchi wa Buyungu wamepoteza imani na NCCR-Mageuzi, hiki si chama cha upinzani tena bali ni kibaraka wa CCM. Mimi sasa nimechukua uamuzi wa kujiondoa kabla hatujaanza kuzomewa,” alisema.
Alipoulizwa ni chama gani atajiunga nacho, mwanasiasa huyo alisema kwa sasa anatafakari kwanza wakati akiangalia chama makini chenye upinznai wa kweli cha kujiunga nacho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment