Uchunguzi uliofanywa katika shule tatu kati ya saba zilizopo kwenye kata hiyo ambayo ipo mjini Namtumbo umebaini kuwa katika shule ya msingi Rwinga wanafunzi 296 wanasomea kwenye vibanda vya miti vilivyoezekwa kwa nyasi .
Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Onesmo Mbawala alisema idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo wanasomea katika vibanda vya nyasi kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa vyumba 12 vya kusomea ambapo vyumba vilivyopo ni vinne tu na kwamba shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1975 ina jumla ya wanafunzi 592.

Wanafunzi wa darasa la awali wapatao 92 shule ya msingi Rwinga wilayani Namtumbo wakiwa darasani na mwalimu wao
Katika shule ya msingi Selous jumla ya wanafunzi 108 wa madarasa ya
tano na sita wanasoma kwenye vibanda vya nyasi hali ambayo walimu
wanasema inachangia kushusha taaluma kwa wanafunzi.
Wanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Selous wilayani Namtumbo wakiwa darasani
Mwalimu wa taaluma katika shule hiyo Sheweji Simba alisema shule
hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007 ina jumla ya wanafunzi 477 huku ikiwa na
vyumba vinne tu vya madarasa kati ya mahitaji ya vyumba nane hali ambayo
imesababisha baadhi ya wanafunzi kusomea kwenye vibanda vya nyasi .Katika shule ya msingi Mkapa ambayo imepewa jina la aliyewahi kuwa kiongozi mkuu wa nchi Rais mstaafu Benjamin Mkapa pia kuna wanafunzi wanaosomea kwenye vibanda viwili vya nyasi kwa kuwa shule hiyo ina vyumba vinne tu kati ya mahitaji ya vyumba nane.

Wanafunzi wa shule ya msingi Mkapa wilayani Namtumbo wakiwa darasani na mwalimu wao
Mkuu wa shule hiyo Hans Mwailima alisema shule hiyo yenye wanafunzi
306 madarasa matatu yanasomea katika chumba kimoja ambapo kuanzia
darasa la tatu hadi la sita wanasomea kwenye vibanda vya nyasi kwa
zamu.“Unajua wanafunzi wana tabia ya kutaniana hivyo endapo darasa moja wakisoma kwenye vibanda vya nyasi kila siku wenzao wanawatania hivyo kukata tamaa na wengine kuwa watoro hivyo tumeamua wote wawe wanasoma kwenye vibanda vya nyasi kwa zamu ili kujenga mvuto wa mazingira ya kusomea’’, alisema.
Mratibu elimu kata ya Rwinga Thomas Komba amekiri shule tatu kati ya saba katika kata yake ambazo ni Rwinga, Mkapa na Selous wanafunzi kusomea katika vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi na kusisitiza kuwa shule za Minazini, Kidagulo, Migelegele na Mandepwende ndizo shule pekee katika kata hiyo ambazo hazina vyumba vya madarasa vilivyoezekwa kwa nyasi.
“Shule zangu tatu za Rwinga,Mkapa na Selous katika kata yangu zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa hali ni mbaya tunafanya jitihada za kuhamasisha jamii ili waweze kujitolea kufyatua tofali kuzichoma kwa kushirikiana na serikali ili kupata vyumba zaidi na kumaliza kero hii ya aibu’’, alisisitiza.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Kasimu Ntara alidai kuwa kuwa kuwepo kwa madarasa yaliojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi katika wilaya hiyo kunatokana na kuanzishwa shule nyingi za msingi.
“Mpango wa uboreshaji wa elimu ya msingi MEM nchini ulisababisha kuanzishwa kwa shule nyingi hivyo baada ya kuondoka kwa MMEM serikali imeshindwa kumudu ujenzi wa vyumba vya madarasa jitihada zinaendelea kufanyika kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa’’, alisisitiza.
No comments:
Post a Comment