KIASI kikubwa cha
fedha hutoroshwa na kufichwa nje ya nchi wakati taifa linapokuwa katika
uchaguzi, vita na matatizo ya kiuchumi.
Uchunguzi wa
Mwananchi Jumapili umebaini kuwa katika mazingira hayo, kuanzia mwaka
1970 hadi 2004, jumla ya Dola 3,899.6 milioni za Marekani, sawa na
takriban Sh6.2 trilioni zimebainika kutoroshwa na kufichwa kwenye benki
za nje ya nchi ikiwamo Uswisi.
Kiwango hicho cha fedha kimezingatia ubadilishaji wa fedha wa Dola moja ya Marekani kwa Sh1,600.
Ripoti ya utafiti uliofanywa na Shirika la Global Financial Integrity,
inaonyesha kuwa kiasi kikubwa cha fedha hizo kilitoroshwa katika kipindi
cha mwaka 1977, 1978, 1985 na 2004.
Kumbukumbu
zinaonyesha kuwa mwaka 1977 ndipo Jumuiya ya Afrika Mashariki
ilipovunjika, mwaka 1978 Tanzania iliingia katika vita vya Kagera dhidi
ya majeshi ya Uganda, wakati huo yakiongozwa na Idd Amin.
Mwaka 1985
ulikuwa mwaka wa uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge ambapo Rais wa Kwanza
wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliondoka madarakani na
nafasi yake kuchukuliwa na Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mwaka 2004 pia
kilikuwa kipindi cha uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge ambapo Rais wa
Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alikuwa akimalizia ngwe yake ya miaka 10
kukaa madarakani.
Uchaguzi huo
uliofanyika Oktoba mwaka 2005 ndiyo uliomwigiza madarakani Rais Jakaya
Kikwete, ambaye kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kitamalizika mwaka
2015.
Katika taarifa hiyo ya Global Financial Integrity, mwaka 1977 Tanzania ilipoteza Dola 539.9 milioni sawa na Sh863.8 bilioni.
Imebainisha kuwa
mwaka 1978, ambapo taifa lilikuwa katika wakati mgumu wa vita na Uganda,
wajanja wachache walifanikiwa kutorosha Dola 635.8 milioni sawa na
Sh1.01 trilioni.
Wakati vita hivyo
vikitumiwa kama mwanya wa kuiba kiasi hicho cha fedha, mwaka 1985
ambapo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliamua kustaafu na Mwinyi kuchukua
madaraka, kiasi cha Dola 1,577.9 milioni sawa na Sh2.5 trilioni
kilitoroshwa.
Taarifa hiyo pia
inaonyesha kuwa mwaka 2004 kipindi ambacho mbio za kuwania urais kwa
ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 zilianza, Tanzania ilipoteza Dola
1,146 milioni (Sh1.8 trilioni) zilizofichwa katika benki za nje ya nchi.
Fedha zinavyotoroshwa
Kwa mujibu wa Shirika la Global Financial Integrity, kuna njia nyingi zinazotumiwa na watu hao kuiba fedha hizo.
Limetaja njia moja kuwa ni kuingiza rekodi mbalimbali kwenye vitabu
husika na maelezo mengine, kutoingizwa kwenye vitabu vya hesabu za
Serikali au mashirika.
Kiasi hicho ambacho huachwa kwa makusudi baada ya kufanyika ujanja wa hesabu, ndicho hufichwa kwenye akaunti za nje ya nchi.
Limetaja pia
biashara za kimataifa kuwa njia nyingine, ambapo, watu hao wasio
waaminifu huongeza bei ya bidhaa au huduma husika na kurekodi hesabu za
bei inayofahamika, huku kiasi kingine kikitoroshwa nje.
Taarifa hiyo
inabainisha kuwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF),
hushindwa kugundua ujanja huo mapema kutokana na taarifa
zinazowasilishwa katika benki hizo kuwa ni zile zilizo kwenye vitabu na
zilizorekodiwa.
Inaongeza kuwa fedha nyingi pia zilitoroshwa baada ya kukosekana kwa taarifa muhimu za masuala mbalimbali ya kifedha.
Katika ripoti
hiyo, imebainika pia kwamba awamu ya nne ya uongozi wa Tanzania ndipo
fedha nyingi zilitoroshwa kwenda nje ya nchi.
Ripoti hiyo
imebainisha kuwa katika kipindi cha utawala wa kwanza ulioisha mwaka
1985, fedha zilizofichwa nje zilikuwa Dola 3,498.3 milioni (sawa na
Sh5.5 trilioni).
Katika Awamu ya
Tatu ya Rais Benjamin Mkapa zilizotoroshwa Dola 2,108.8 milioni (Sh3.3
trilioni), wakati katika Awamu ya Pili ya Mzee Mwinyi zilitoroshwa Dola
529.1 milioni (Sh846 bilioni).
Utafiti huo pia unaonyesha pia nchi 20 za Afrika zinazoongoza kuficha fedha nje huku Nigeria ikiwa kinara.
Jumla ya Dola za Marekani 1.8 trilioni zimefichwa katika benki
mbalimbali nje ya nchi kutoka nchi za Kiafrika katika kipindi cha mwaka
1970 hadi 2009.
Akizungumzia
suala hilo, Naibu Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya alisema Serikali
inatambua uwepo wa tatizo hilo na tayari imeanzisha mikakati ya
kukabiliana nalo.
Alisema kuwa
Wizara ya Fedha imeanzisha kitengo maalumu kiitwacho Financial
Intelligence Unit, ambacho pamoja na mambo mengine kitashughulikia
utoroshwaji wa fedha nje ya nchi.
“Suala hilo
tumeliwekea mikakati na tayari tumeshaanzisha kitengo kinachoshughulikia
suala hilo, tunachohitaji ni kuongeza nguvu kazi kwa sababu inahitajika
watu wenye uzoefu mkubwa,” alisema naibu waziri huyo.
Alifafanua kuwa
kitengo hicho kitafanya kazi Tanzania Bara na Visiwani na kuongeza kuwa
sheria ya kuzuia fedha haramu itaanza kutekelezwa hivi karibuni, akisema
kuwa anaamini itasaidia kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza kwa
njia ya simu, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Delfin
Rwegasira alisema kuwa chanzo kikubwa cha watu kutorosha fedha nje ya
nchi ni kukosekana kwa uwazi na ufisadi.
Alifafanua kuwa
tangu kuanza kwa mfumo huru wa kiuchumi, kumekuwa na wafanyabiashara
waliotumia mianya ya uhuru wa kiuchumi kukimbiza fedha hizo.
“Sidhani kama
nchi kuwa katika misukosuko kunaweza kuwa chanzo cha utoroshwaji wa
fedha, chanzo kikubwa ni kukosekana kwa uwazi na rushwa,” alisema Dk
Rwegasira.
Aliongeza kuwa
kutoroshwa kwa fedha nje ya nchi kunaweza kutokea pale wafanyabiashara
wanapokuwa na shaka na biashara zao au mustakabali wao katika nchi,
hivyo ili kuhakikisha hawapati matatizo kiuchumi huanza kukimbiza fedha
zao nje ya nch.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment