Soma uozo wa wabunge wa CCM...Mwigulu na Komba

MWIGULU

MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa
nafasi hii ili nizungumze na Watanzania. Awali ya yote, Watanzania wanatakiwa wawe makini
sana na waigizaji. Ukimpata mwigizaji mzuri, unaweza ukalia, kumbe mwenzio anaigiza na hiki
ndicho ambacho kimetokea muda mfupi uliopita hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa...
MWENYEKITI: Mheshimiwa, nakuomba ufute neno uigizaji.
WABUNGE FULANI: Aaah!
MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta kama kuna waigizaji hapa.
MWENYEKITI: Naomba ufute neno uigizaji.


MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafuta neno uigizaji kama kuna
waigizaji, lakini maana ya kusema hivi ilikuwa ni hii, tatizo linalojitokeza hapa ni kwamba, bajeti
imeandaliwa na wataalam, lakini watu badala ya kuuliza wajue undani wa bajeti, aliyesomea
Sheria za Mambo ya Kichawi na yeye anakuwa mchambuzi wa uchumi, mwenye uzoefu wa
kuendesha disko anakuwa mchambuzi wa uchumi, unawachanganya Watanzania. Sasa uhalisia
ndio huu, mimi ni Mchumi wa Daraja la Kwanza na Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania, ngojeni
niwaambie uhalisia wa bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano,
tunapoongelea 35%, tunajumuisha pamoja na uwekezaji kwenye sekta ya elimu lakini
tunapozungumzia bajeti hii ya leo, sekta ya elimu iko pembeni, fedha zake zimewekwa pembeni,
zile za maendeleo zimewekwa pembeni. Watanzania tuulizane, hivi kweli tunaposomesha
wanafunzi vyuo vikuu, hatuwekezi? Hivi kweli tunapojenga maabara, hatuwekezi? Hivi ni kweli
tunaposomesha vyuo, tunapoandaa Wataalam wa Ugani, tunapoandaa Madaktari, hatuwekezi?
Tulisoma wapi? Hiyo Sheria iliyokuwa inatenga investiment on human capital, ilikuwa ni ya miaka
ya 50 na 60 lakini ukisoma David Roma, ukasoma Waive, ukasoma Mankyu, miaka ya 90, Cop
Douglas Production Function, inatambua human capital kama investiment. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mpango wa Maendeleo huu tunaojadili, umejumuisha
investiment on human capital ndio ukapata 35%. Ukienda kwenye bajeti ya mwaka huu,
ukichukua investiment kwenye elimu, uwekezaji tuliouweka kwenye elimu, bajeti ya maendeleo
inaenda 39% kwenda 40%. Mmesoma wapi nyie? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, ukiingalia kiutaalamu tu bajeti yenyewe, kiutaalamu
tu, dependency ratio, utegemezi bajeti imepungua. Ukiweka na ile mikopo kwa sababu mikopo
nayo ni fedha yetu tutalipa, ukiondoa na ile ya mikopo, utegemezi kwenye bajeti imebaki 6.5%.
Sifa nyingine ya bajeti, ukienda zile fedha zinazoenda kwenye kulipa mishahara, hamna hata senti
moja inayoenda kwenye mishahara, mishahara inalipwa na fedha za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu muone sasa hili nililolisema ambalo mmesema nilifute, hebu
oneni sasa Bajeti ya Kivuli, wameandika kwamba, kima cha chini kitakuwa 315,000/= hawajui
wanaolipwa kima cha chini ni wangapi, zidisheni mpate hesabu, mimi nitawaambia mwishoni.
Halafu chukueni Walimu muwapandishie mishahara mara 50, chukua Madaktari uwapandishie
mara 50, chukua Manesi uwapandishie mara 50, tafuta jumla yake. Halafu chukua walewale,
makundi matatu haya, uwapandishie mara moja na nusu, bajeti ya matumizi inaenda zaidi ya hii
shilingi bilioni tisa waliyoandika wao. Hii waliyoandika kwenye matumizi ya kawaida inazidi,
ukijumlisha na ile wanayosema kwamba watalipa pensheni kwa wazee, hawajui idadi ya wazee,
ukijumlisha inakuwa zaidi ya shilingi trilioni 15, mmnatumia bajeti ya wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu wanasema...
MBUNGE FULANI: Silly thinking.
MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi hili nitalirudia tu, halafu
wanasema kujenga, wanasema kupunguza mzigo wa matumizi ya magari. Mwaka jana
Mwenyekiti wao, Mheshimiwa Mbowe, alirudisha gari akisema kwamba, kupunguza matumizi,
akawahadaa Watanzania. Baada ya muda fulani, kumbe alilikataa lile gari kwa sababu
limechakaa, lilikuwa linatumiwa na Kiongozi aliyepita, baada ya muda fulani kachukua
kimyakimya gari lingine analitumia. Amelirudisha kimyakimya hajawaambia Watanzania kama
ameshalichukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu wanatakiwa kwa kweli Wachamungu wote, mimi
tangia nizaliwe sijawahi kuona Kambi ya Upinzani yenye pepo mtaka vyeo kama hawa hapa.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanatakiwa waombewe, watalipeleka Taifa pabaya, mimi
nawaambia Watanzania mkiendelea kushabikia watu ambao haijulikani kama wako normal au
wanatakiwa wawe Mirembe mtapata kiongozi kama Iddi Amini hapa.


MBUNGE FULANI: Mwongozo wa Spika!
MBUNGE FULANI: Mwehu huyu!
MBUNGE FULANI: Mwongozo! Anatutukana huyu!
MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Nimesema niseme na Watanzania, ngojeni niwaambie,
jambo lingine ambalo wanalolikataa hapa, ngojeni mjue unafiki uko wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine wanalolikataa wanaongelea OC kama vile ni
dhambi kubwa kwelikweli, angalieni OC kuna nini, OC Serikali imetenga shilingi bilioni 140 kupeleka
vijana JKT, hivi kweli hiyo ni dhambi kupeleka vijana JKT. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Waambie!
MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Serikali imetenga OC kwenda kwenye Tume ikakusanye
maoni ya Katiba Mpya, mnataka Katiba Mpya hamtaki tuweke bajeti, mnataka Katiba mpya kwa
kutumia fedha gani.
MBUNGE FULANI: Mwongozo wa Spika!
MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Serikali imetenga fedha kwenye OC kwa ajili ya sensa,
mnataka sense, hamtaki tuweke bajeti. Serikali imetenga fedha kwenye OC kwa ajili ya fidia za
watu wanaondolewa kwenye maeneo kupisha miradi ya maendeleo, mnataka zisiwekwe, wale
watu mtawapatia hela gani mnapowaondoa pale? Serikali imetenga fedha kwenye OC kwa ajili
ya chakula, wanafunzi, wafungwa, wagonjwa mnataka ziondoke mtawapa nini? (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mwongozo wa Spika!
MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Mimi sijawahi kuona Bajeti Kivuli ya aina hii, this is concisely
and precisely rubbish. (Makofi)
MWENYEKITI: Samahani kaa chini, Mheshimiwa naomba ukae.
MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
(Kicheko/Makofi/Vigelegele)
MWENYEKITI: Ngojea Mheshimiwa Mwigulu, order in the House, Mheshimiwa Mwigulu
naomba ufute neno pepo kwa sababu ni kinyume…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizomea)
MWENYEKITI: Order in the House.
MBUNGE FULANI: Mbona walipotaja Mungu mpya hukusema?
MWENYEKITI: Order in the House.
MBUNGE FULANI: Afute.
MWENYEKITI: Order in the House, naomba ufute neno pepo halafu tuendelee.
MBUNGE FULANI: Mwongozo!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwigulu futa neno pepo tuendelee.
MBUNGE FULANI: Mwongozo wa Spika!


MHE. MWIGULU L. M. MADELU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa humu ndani nafuta lakini watu
wa aina hiyo wakaombewe, nafuta neno hilo. (Makofi)
MBUNGE FULANI: Mwongozo wa Spika.
MWENYEKITI: Naomba tuendelee.
MBUNGE FULANI: Kuhusu utaratibu!
MWENYEKITI: Naomba tuendelee, sasa namwita Mheshimiwa Ahmed Ally Salum na
Mheshimiwa Amina Clement ajiandae na atafuatia Mheshimiwa Komba. Yupo au hayupo?
MBUNGE FULANI: Yupo!




KOMBA


MWENYEKITI: Ahsante, namwita sasa Mheshimiwa Amina Clement na wa mwisho atakuwa
Mheshimiwa Capt. John Komba.
MHE. CAPT. JOHN D. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nishukuru kwa kunipa nafasi
nichangia bajeti hii.
Kwanza nikuambie mimi nafikiri moja ya masharti ya kuingia humu ndani tuwe tunapimwa
akili kama wote tuna akili sawasawa au namna gani, inawezekana watu waliambiwa waende
Mirembe halafu waje humu, wameanzia humu kabla ya kwenda Mirembe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili litajirudia sana maana huwezi kusema kila mwaka
tunashuhudia upuuzi humu ndani, tunapanga bajeti ya upuuzi humu ndani, mwaka jana upuuzi,
mwaka huu upuuzi na yeye yumo humuhumu ndani, anakaa humu, huu ni wendawazimu kabisa.
Ni vizuri tukapimana akili kidogo wa Mirembe wakaenda Mirembe, halafu wakarudishwa hapa
wakawa wamesharekebishwa katika ugonjwa.
MBUNGE FULANI: Tuanze na wewe.
MHE. CAPT. JOHN D. KOMBA: Maana yake inapotukanwa, hapa hakitukanwi chama
chochote hapa, lakini mtu anaposimama anazungumza habari jamani wananchi acheni CCM,
hii siyo kampeni humu ndani, humu tujadili habari ya bajeti hii. Kama ulishindwa kupata watu
wengi huko ulikotoka miaka miwili iliyopita wananchi wale ndiyo wameipa CCM ridhaa ya
kutawala miaka mitano, sasa unapowatukana wananchi wale mimi ndiyo nauita ukichaa. Kwa
hiyo, ni vizuri watu wakapimwa kwanza kabla hawajaingia humu ndani. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naangalia sana hizi TV za nje, UBC ya Uganda, KBC ya
Kenya, naangalia Wabunge wa Uganda na wa Kenya wanaisifu bajeti yetu tumejali wanafunzi,
tumejali barabara, tumeleta matrekta wanayaona na wanaizungumza kila siku lakini sisi
tunaiponda hiyo bajeti halafu tunasema bajeti yetu ni kujirudia mwaka hadi mwaka. Ni lazima
irudiwe kwa sababu sisi kazi yetu ni kusaidia wananchi lazima tuwasemee wananchi jana, kesho,
kesho kutwa tutawazungumza tu, wanafunzi watazungumzwa mwaka jana, mwaka huu, mwakani
kwa sababu ndiyo lengo la kuwakomboa wanafunzi na wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nimeitwa ghafula niende kwenye Jimbo langu,
Jimbo langu ni maskini...
WABUNGE FULANI: Ohoo! Hapohapo.
MHE. CAPT. JOHN D. KOMBA: Jimbo langu ni maskini, katika Wilaya ya Mbinga, lile Jimbo
ambalo limetengwa ndiyo Jimbo maskini, lakini bahati mbaya sana wenzetu wanaofanana na sisi
wa Malawi ndiyo wanaozalisha samaki kupeleka nje, ziwa lilelile huku hakuna samaki lakini
upande ule wanazalisha samaki, wanapaki kwenye makopo wanapeleka nje. Mimi silaumu sana
Serikali yangu kwa sababu Malawi ni nchi ndogo sana, Malawi inaingia kwenye nchi yetu zaidi ya
mara kumi, kwa hiyo, katika nchi wengine walipendelewa mapema, watu wa Kaskazini walipata,
watu wa katikati walipata, mashariki walipata sasa bajeti hii ilenge sisi watu wa pembezoni kama
ambavyo Mheshimiwa Rais amekuwa akizungumza siku zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa kule Mbinga Magharibi kule ama kule Nyasa
tunategemea bandari ya Bambabay, lakini ukiangalia bandari ya Bambabay haijapewa pesa
hata senti tano sasa maendeleo yatakujaje? Kama unatengeneza bandari ya Mtwara unataka
bidhaa ziende Malawi, Zimbambwe, Botswana, Namibia, South Afrika, Kongo, zitakwendaje kama
bandari ya Bambabay haiwezi kupitisha mizigo hiyo? Kwa hiyo, naomba sana bandari yetu ya
Bambabay ipewe umuhimu wa kwanza kama zilivyo bandari zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa letu la Nyasa, ni Ziwa ambalo vifaa vyake ni duni na kwa vile
sisi tulikubali kuwasaidia watu wa Kaskazini tulikuwa tunawalimia mashamba, maana tunalima
mahindi wanakula wao, tunalima maharage wanakula wao, tunalima mchele wanakula wao,
sasa ni wakati wa kusaidia watu wale waweze kuvua vizuri samaki ili wale vizuri, tena na hao
tunawapelekea maana samaki wako, vyombo vya kuvulia ni duni, teknolojia ni duni. Tunaomba
sana bajeti hii ilenge kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo wanaokaa kandokando ya Ziwa Nyasa
na pia na maziwa mengine kwa mfano Rukwa, Tanganyika, Nyumba ya Mungu wapi wasaidiwe
hao, maana tumeshawasaidia sana Ziwa Victoria, kila siku, maana hata siku hizi nikiangalia
wanavyotoa habari ya hali ya hewa wanazungumza halafu wanasema Ukanda wa Ziwa, hivi sisi
Tanzania tuna Kanda moja tu maana yake ni Ziwa Victoria basi uko Ukanda wa Ziwa Victoria,
Ukanda wa Ziwa Nyasa, Rukwa haya maziwa haya nayo yana ukanda wa ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba sana kutukanana tukuache, maana yake
tumeshaona huko katika Mabunge mengine watu wanapigana ngumi, sasa huku tunakoenda
tutapigana ngumi na ngumi zilizo upande huu ni nyingi kuliko za upande huu mtakufa. Kwa hiyo,
naomba sana heshimu chama cha wenzako, heshimu chama kilicho madarakani, heshimu
wananchi waliotoa madaraka hayo, changia hoja yako, vunja hoja iliyoko siyo kutakana Chama
cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na uwe unaangalia pande zote wanaotukana
sana hawa uwaambie ndiyo watoe maneno, lakini yule uliyemwambia atoe neno lile neno halina
sababu ya kulitoa. Wanaotukana hawa ndiyo uwaambie, naunga mkono hoja mia kwa mia.

No comments:

Post a Comment