MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa,
Freeman Mbowe, leo anatarajia kuongoza harambee ya kukusanya fedha kwa
ajili ya kufanikisha mkakati wa vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika jiji
la Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, mjumbe wa
Kamati Kuu na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema
harambee hiyo itafanyika kuanzia majira ya saa 1:00 usiku katika Hoteli
ya Serena kwa lengo la kuwakutanisha wanamabadiliko wa daraja la kati.
Alisema katika harakati za vuguvugu la mabadiliko wana lengo la
kukusanya kiasi cha shilingi bilioni tano kwa upande wa Dar es Salaam,
wanatakiwa kukusanya asilimia kumi ya fedha hizo.
“Tulienda Mwanza pamoja na mwenyekiti na tulifanya hivyo, kuna dalili
za mafanikio makubwa na kama watu watakuwa makini, basi kutakuwa na
mafanikio na lengo la fedha hizo ni kununulia magari kwa ajili ya
kuendesha kampeni nchi nzima,” alisema Lema.
Naye Mwenyekiti wa M4C mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mayunga, alisema
wameandaa chakula cha jioni ambapo watu 500 kutoka katika kada tofauti
tofauti, wamealikwa.
Alisema lengo lingine ni
kukusanya rasilimali watu, fedha na vifaa vya kazi kwa lengo la kueneza
chama katika vitongoji na mitaa ambako ndiko kunakoakisi maisha halizi
ya Watanzania.
Alitaja lengo lingine kuwa ni
kuweka mkakati wa kuendeleza mshikamano na umoja miongoni mwa
wana-mabadiliko wa daraja la kati ili kutoa mchango kwa mabadiliko ya
katika jamii.
Alisema, wanahakikisha chama
kinakusanya rasilimali fedha kwa lengo la kununua vitendea kazi kulipa
gharama za kupata rasilimali kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa
serikali za mitaa mwaka 2014 na uchaguzi mkuu mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment