CHAMA Cha
Mapinduzi(CCM) kimemtaka Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe
kuwataja hadharani wabunge 70 kutoka na mawaziri saba wa CCM, ambao
wameomba kujiunga na chama hicho cha upinzani ili kuuthibitishia umma
kama alichochokisema kina ukweli.
Juzi, akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja
vya NMC, Unga Ltd jijini Arusha, Mbowe alisema idadi hiyo ya wabunge na
mawaziri wanatarajia kujiunga Chadema siku za usoni na kutangaza chama
hicho tayari kimevuna wanachama 10,400 kwa mkoa wa Arusha na Manyara.
Wanachama hao ni kutoka Ngorongoro (2,500), Monduli (2,000), Longido
(800), Arumeru (1,200) Arusha mjini (2,600) na Simanjiro (1,300).
Jana, akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema kama Mbowe ana uhakika na anachokisema ni bora
angesubiri kitokee halafu ndiyo azungumze vinginevyo awataje wanachama
hao ili umma umuamini."Anachokizungumza hakina msingi na hoja zake
hazina mashiko.
Anachokizungumza angekaa nacho kwanza ili kitokee na hivi sasa wananchi
wa Arusha wana matatizo hawahitaji kujua na nani anatoka wapi na kwenda
wapi," alisema Nape.Alisema chama makini hakiwezi kujitangaza kuwa
kinachukua wanachama wa chama kingine, bali ni kutafuta wanachama wapya
kwani Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40.
"Ninamshauri Mbowe aache kukurupuka na aache uongo, awataje hao
anaowazungumzia na akiendelea na tabia ya aina hii itamshushia
heshima,"alisema Nape na kuongeza;"Siasa za aina hii amuachie Dk Slaa
kwani Mbowe yeye ni mwenyekiti wa chama na kiongozi wa kambi ya upinzani
bungeni anaheshimika.
"Nape alisema ni muhimu Mbowe akaacha kukurupuka kwa kutoa hoja bila
mpangilio kwani heshima aliyonayo itashuka akiendelea na hali hiyo.Juzi
mbowe alitumia mkutano huo kuwatoa hofu wana Chadema wanaotilia shaka
wimbi la viongozi na wana CCM wanaojiengua na kujiunga na chama hicho
kikuucha upinzani kuwa Chadema iko imara na hakiwezi kuhujumiwa wala
kupenyezewa mamluki kama baadhi wanavyodhani.
Mbowe alitamba kuwa ameongoza harakati za upinzani kwa zaidi ya miaka 20
sasa, ambayo imeanza kuzaa matunda kwa Watanzania kukiamini Chadema
hivyo hawezi kukubali kuruhusu mtu yeyote yule anayetumia njia ya wazi
au ya kificho kukidhoofisha.
Nassari, Heche matataniKatika hatua nyingine, jeshi la polisi mkoani
Arusha linawasaka kwa mahojiano mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha),
JohnHeche kuhusiana na kauli walizotoa kwenye mkutano huo wa hadhara
uliofanyika juzi kwenye uwanja wa Unga LtD.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya jeshi la polisi na baadaye
kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa
zimeeleza kuwa kwenye orodha hiyo ya viongozi wanaosakwa pia yumo
aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Ally Bananga aliyehamia Chadema hivi karibuni.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Kamanda Mpwapwa alisema viongozi hao
walitoa maneno yanayoelekea kuwa ya uchochezi ambayo hayawezi kuachwa
bila wahusika kuhojiwa kujua walichomaanisha.
“Kwani wewe hukuwepo pale uwanja jana (juzi) wakati viongozi wa Chadema
walipokuwa wakihutubia? Walitoa maneno ambayo lazima tuwahoji
kujiridhisha walichomaanisha na hili ni jukumu la kawaida la kiuchunguzi
la polisi,” alisema Kamanda MpwapwaKaimu Kamanda huyo ambaye
amaeteuliwa kuwa Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara katika uteuzi na
mabadiliko yaliyofanywa juzi na Inspekta Jenerali wa polisi nchini
(IGP), Said Mwema alisema hatua zaidi dhidi ya viongozi na mwanachama
huyo mpya wa Chadema itajulikana baada ya kuhojiwa.
“Siwezi kukanusha wala kuthibitisha iwapo tutawafungulia mashtaka kwa
kauli hizo tunazozichunguza, uamuzi utategemeana na maelezo yao na
taarifa za uchunguzi tunazoendelea kukusanya,” alisema Mpwapwa.
Katika mkutano huo wa hadhara, viongozi kadhaa wa Chadema walioongozwa
na Mbowe walihutubia na kutoa kauli mbalimbali huku Nassari akitumia
fursa hiyo kuzungumzia utendaji wake ndani ya bunge mara alipoapishwa
baada ya kuibuka mshindi katika uchaguzi mdogo uliofanyika Aprili Mosi,
mwaka huu.
Mbunge huyo kijana aliueleza umati mkubwa uliohudhuria mkutano huo
uliolenga kuzindua oparesheni ‘Vua gamba, vaa gwanda’ kuwa jeshi la
polisi linapaswa kuongeza juhudi katika upelelezi na uchunguzi wa mauaji
wa aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, Kata ya USA-River, Msafiri Mbwambo
aliyechinjwa kwa nyuma na kitu chenye ncha kali.
Nassari alisema uvumilivu wa wana Chadema kuendelea kusubiri kwa muda
mrefu uchunguzi wa mauaji hayo ya kinyama unakaribia kufikia kikomo kwa
sababu wauaji walitumia simu kumwita marehemu hivyo, ni rahisi kwa
vyombo vya dola kufuatilia namba hiyo na kutambua wahusika kirahisi.
Pengine kauli inayowezekana kumponza hadi kuitwa kwa mahojiano polisi ni
madai yake kuwa iwapo vyombo vya dola na serikali vitaendeleza
ukandamizaji dhidi ya wanaopigania haki, usawa na ustawi wa jamii kama
inavyoshuhudiwa sehemu mbalimbali nchini, basi watatangaza Arusha kuwa
eneo linalojitegemea yeye akiwa Rais na aliyekuwa mbunge wa Arusha
mjini, Godbless Lema akiwa Waziri Mkuu.
Hata hivyo, Mbowe alifuta kauli hiyo aliposimama kuhutubia akisema
Chadema inahitaji kuunganisha na kukomboa nchi yote bila kuacha kipande
chochote akisema kauli ya Nassari ilitokana na hamasa ya kisiasa
jukwaani.
Kwa upande wake, Bananga yeye alitumia fursa hiyo kuwaomba radhi wana
Chadema wote aliowakwaza kwa vitendo vyake alipokuwa CCM na papo hapo
akamshukuru Rais Jakaya Kikwete na mtoto wake, Ridhwani kwa kile
alichodai kukamsirisha na kumpa mwanya wa kufikiri sawa sawa na kujiunga
Chadema alichogundua ndicho chama chenye dhamira ya kweli ya kukomboa
taifa.
Heche yeye aliueleza umati huo kuwa ataanza oparesheni hiyo katika mikoa
ya Kusini kwa lengo la kukisambaratisha CCM na kukiimarisha Chadema
huku akisema, Rais Kikwete ameonyesha dharau kubwa kwa umma
unaolalamikia maisha magumu na kupanda kwa gharama za maisha kwa
kuzidisha ukubwa wa baraza la mawaziri kwa kuteua mawaziri watano zaidi
ya waliokuwepo awali.
Katika hatua nyingine, maelfu ya wakazi wa Karatu, jana walijitokeza
kumpokea Mbunge mteule wa viti maalum wa Wilaya ya Karatu, Cecilia
Pareso.Pia katika mkutano huo, Chadema walitoa tamko la kuitaka Serikali
kuwafikisha mahakamani mawaziri wote waliondolewa kutokana na
ubadhirifu la sivyo chama hicho, kitaandaa maandamano yasiyo na ukomo
nchi nzima.
Mjumbe wa Kamati Kuu Godbless Lema alisema haiwezekani mawaziri
wabainike wamesababisha upotevu wa fedha za zaidi ya Sh9 trilioni,
wakaondolewa uwaziri tu huku mamia ya watu ambao wametuhumiwa kwa wizi
wa simu wanaozea magereza. “Tunasema hivi, hawa mawaziri wote
waliobainika kusababisha hasara kwa taifa lazima wafikishwe kwenye
vyombo vya sheria na kuvuliwa ubunge,” alisema Lema.
Alisema Sh9 trilioni zinatosha kutengeneza barabara za lami katika
mikoa yote nchini, au kujenga nyumba za walimu wote wa shule za
sekondari na msingi.
No comments:
Post a Comment