Mwigamba: Namshukuru Mungu kutuletea Rais Kikwete

Samson Mwigamba
NAJUA msomaji unajiuliza maswali mengi ndani ya sekunde chache za kusoma kichwa cha habari cha makala yangu ya leo.
Mojawapo ya swali muhimu unalojiuliza ni kama hii kweli ni Kalamu ya Mwigamba ndiyo inamshukuru Mungu kwa kutupatia Kikwete kuwa rais wetu ama mhariri amechanganya kurasa akachapa makala ya Nape Nnauye kwenye ukurasa wa Kalamu ya Mwigamba.
Lakini kama msomaji ni mfuatiliaji wa karibu wa makala zangu na kama utakuwa na kumbukumbu nzuri utakumbuka kuna siku huko nyuma niliwahi kuandika makala nzima ya kukubali kwamba ni kweli JK alikuwa chaguo la Mungu.
Niliwahi kukubaliana na Baba Askofu Methodias Kilaini aliyetamka mwaka 2005 kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwamba Kikwete alikuwa ni chaguo la Mungu. Nilisema huenda mwaka 2005 hatukumwelewa Baba Askofu Kilaini.
Nikasema kwamba nakubaliana naye kama alisema JK ni chaguo la Mungu akimaanisha ni tatizo lililoletwa kwa watanzania ili wajifunze kubadilika. Tunasoma katika Biblia kwamba pale wana wa Israel walipoamua kwamba sasa hawataki kuchaguliwa mfalme na Mungu wanataka wachague wenyewe, Mungu aliwaongoza kumchagua mfalme aliyeitwa Sauli.
Sauli hakuwa kiongozi mzuri, akalipotosha taifa na kutenda maovu mbele za Bwana na wananchi wakaingia katika shida kubwa mpaka wakajuta kumchagua.
Bwana akamchagua JK ili aje kumtumia kuwaokoa Watanzania hawa maskini. Biblia inasema “akawauza kwa adui zao” nao wakazama na kummwagia JK ushindi wa asilimia 80 ambayo haijapata kupatikana katika uchaguzi wa vyama vingi siyo hapa kwetu tu bali hata katika nchi nyingi zenye demokrasia inayoeleweka.
Wapo waliosema huyu ndiye tuliyemsubiri. Kina Prince Bagenda waliofikia kuandika kitabu kwamba ‘JK ni tumaini lililorejea’ hawakukosekana.
Lakini alipoanza kutawala haikuchukua muda kugundua kwamba Watanzania tumechagua Sauli kuongoza nchi. JK ameprove kuwa rais dhaifu kuliko wote waliopita kiasi cha kufikia wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kusema nchi ina ombwe la uongozi. Si maneno yangu ya wazee wenye maono kama kina Joseph Butiku na Joseph Warioba.
Ni rais pekee ambaye ameonyesha kwamba Waziri Mkuu wake anaweza kutuhumiwa kila kona ya nchi lakini akasubiri mpaka ripoti ya kamati teule ya Bunge ije imuumbue ndipo amshauri kujiuzulu na si kumtimua.
Mzee Mwinyi aliposoma tu kitabu cha Nyerere kilichomtuhumu Malecela akiwa waziri mkuu wakati huo na mzee Kolimba akiwa katibu mkuu wa chama wakati huo, alichukua hatua mara moja akavunja Baraza la Mawaziri na kumtangaza Msuya kuwa waziri mkuu mpya.
Mzee Mkapa aliwashauri mawaziri wake wenye tuhuma wajiuzulu mara moja akina Simon Mbirinyi, Hans Kitine, Idd Simba, nk. pale walipotuhumiwa. Lakini hilo huwezi kulisikia wakati wa Kikwete badala yake utasiki waziri kwa jeuri akisema siwezi kujiuzulu kamwe labda rais anifukuze. Naye rais hutasikia akimfukuza waziri.
Tumeyasikia maneno hayo kwa Hussein Mwinyi wakati akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, baada ya mabomu ya jeshi kuangamiza watu Mbagala na Gongo la Mboto, tumeyasikia mara kadhaa kwa Maige, tumeyasikia kwa Ngeleja, na wengineo wengi na juzi hapa tumeyasikia mpaka yakawa yanakereketa masikioni kutoka kwa Omary Nundu.
Maskini wakati huu wa Kikwete wameongezeka kuliko kawaida, rushwa ya kupindukia imeanza kusikika wakati huu wa Kikwete na ni wakati huu wa Kikwete ambapo msamiati wa ufisadi tuliokuwa tunausikia tu huko Kenya, umeshika kasi hapa kwetu.
Mauaji ya raia kwa vyombo vya dola yameongezeka sana wakati huu wa Kikwete. Huko nyuma tulizoea kutangaziwa mara kwa mara majambazi yameua watu wangapi. Siku hizi ni kawaida kusikia polisi wameua watu wangapi.
Nchi wakati huu wa JK imepoteza mwelekeo. Wazee wa CCM, wala si wa upinzani, wanapiga kelele kila kukicha. Akina Warioba, Kaduma, Butiku, Kitine na wengineo lakini wanajibiwa kwa kejeli na serikali ya Kikwete na awamu mpya ya secretariat aliyoiweka kwenye chama chake.
Ni vigumu leo kujua nini kitatokea kesho kwenye serikali hii ya Kikwete. Kila mtu ni gamba, kila mtu ni fisadi na kila mtu ni mpiganaji dhidi ya ufisadi.
Sasa wananchi wameshtuka. Wametambua kwamba anapwaya na siyo yeye peke yake bali wote waliobaki ndani ya chama hicho kikuukuu.
Ni Kikwete alipambwa akapambika, akaonyeshwa kama masalia pekee aliyebaki ndani ya CCM mwenye uwezo wa kulinyoosha taifa kuelekea tunakotaka. Watanzania waliaminishwa wakati ule kwamba hakuna aliyebaki ndani ya chama hicho anayestahili kuchukua uongozi wa nchi zaidi yake yeye.
Kwa hiyo alipokuja kuvurunda wananchi wakasema basi inabidi CCM iondoke madarakani. Kwa sababu waliambiwa ni JK peke yake aliyebaki kwenye CCM, sasa kama amechemsha tena vibaya kiasi hiki CCM itasema nini kuwashawishi Watanzania kwamba kuna mwingine tena zaidi ya Kikwete? Najua waliotengeneza huo mkakati walikuwa na mawazo yao kichwani lakini nawaambia imekula kwao.
Nawapongeza sana CHADEMA. Ni chama kinachojua nini kinafanya na nini lengo lao. Wako tayari muda wote kutumia kila nafasi itakayojitokeza mbele yao kuzidi kuisogelea Ikulu. Huko nyuma niliwahi kusema maneno haya na leo nayarudia. Mwaka 2005 Mungu alifanya machaguo mawili.
Alimchagua JK kuiangamiza CCM na akamchagua Slaa kuinyanyua CHADEMA. Ndiyo maana wakati fulani nikasema, wote, JK na Slaa, ni machaguo ya Mungu.
Saa ya ukombozi imewadia. Wakati wa kuiondoa CCM madarakani umewadia. Wanaohusika na kuiondoa CCM madarakani ni Watanzania wote wakiwamo Wana CCM wengi.
Operesheni inayokuja kumaliza kazi ni hii ambayo CHADEMA wameipachika jina la M4C, kwa kirefu ikiwa ni “Movement For Change” yaani “Vuguvugu la Mabadiliko”.
Kupitia M4C Watanzania wanafikishiwa elimu ya uraia na kufumbuliwa macho wajue haki zao za kidemokrasia, wajue nguvu waliyonayo kama chanzo pekee kwa mujibu wa katiba yetu cha mamlaka wanayopewa serikali.
Wananchi wa kawaida wanafundishwa kuelewa kwamba wana nguvu kubwa mno iitwayo nguvu ya umma ambayo wakiitumia vizuri hakuna mtawala wala mwanasiasa wala vyombo vya dola vitakavyoweza kuwanyanyasa.
Wananchi wanajua kupitia M4C kwamba hatupaswi kuchukua silaha za jadi kupambana kuiangusha serikali, kwamba hatuna haja ya kuipigia magoti CCM kila kukicha na kuiomba iisimamie serikali yake iwatumikie wazawa na si wageni.
Si lazima tuibembeleze serikali ya CCM itujengee barabara na zahanati nasi tuishukuru kama vile wametoa msaada wa wahisani. Kwamba si lazima tukakae vikao na wenye migodi kuwaomba kwenye matrilioni ya pesa wanayoyapata kwenye dhahabu yetu, almasi yetu, tanzanite yetu na madini mengine mengi, eti watoe kwa mwaka vimilioni 200 tu kwa halmashauri ya wilaya ama mji inayopakana na mgodi ambayo mgodi umo kwa ajili ya kutengeneza madawati ya kukalia watoto wetu.
Nguvu tuliyonayo twaweza kuisubirisha siku ya kuandikisha kupiga kura na siku ya kupiga kura. Tujiandikishe kwa wingi na siku ya kura tupige kwa wingi kuiondoa CCM madarakani. Tufanye kama Arumeru Mashariki. Mpaka CCM wanapigia CHADEMA wanapigia mabadiliko lakini wakiwa ndani ya CCM.
M4C inalenga kukusanya pesa kwa viwango vya mia mia, elfu elfu, elfu kumi kumi, elfu hamsini hamsini, laki laki na kadhalika. Hizi hela ni kidogo sana lakini tukichanga sisi maskini tulio wengi zitatutosha kujenga chama mbadala nchi nzima na kukiwezesha kufanya kampeni za kistaarabu lakini kabambe hapo mwaka 2014 na 2015 kuchukua dola.
M4C inalenga kujenga mtandao wa chama nchi nzima. Mwaka huu mwezi wa ujao utaanza uchaguzi kwenye ngazi za misingi na mabalozi wa nyumba kumi. Shiriki kutandaza chama kote nchini. Arusha kama kawaida yetu tutaset mfano hivi karibuni. Tunawasihi watakaoona mkakati wetu unafaa wauige lengo ni kufikia mabadiliko na si nani alianzisha nini.
M4C inalenga kuwaleta nyumbani makamanda waliopotea jangwani. Wakati fulani palikuwa na jangwa tupu (CCM), hamkuona malisho mabichi. Kwa hiyo miaka yote mmekuwa mkijua hamna zaidi ya majani makavu. Mlipoanza kuona majani mabichi mlidhani yana sumu, haiwezekani nchi hii kukawa na malisho mazuri kiasi hiki.
Hapana, msimsikilize shetani ambaye kazi yake ni kuwakatisha tu tamaa. Njooni ndani ya zizi lenye mchungaji mwema. Mkono wa kuume wa M4C ni operation ndogo inayoitwa “Vua gamba, vaa gwanda”. Mpaka sasa karibia makamanda elfu 20 wamejiengua kwenye magamba na kuvalia magwanda.
Hilo nalipongeza sana na hatimaye unabii unaelekea kutimia. Lakini naipenda sana operation ndogo nyingine ya M4C ambayo naweza kuiita mkono wa kushoto wa M4C. Hii ni operesheni ya kimya na kwa kweli naipenda kwa kuwa iko effective kuliko zote. Nayo ni “Toa gamba moyoni, valia gwanda moyoni”.
Hii kwa sasa imefikisha mamilioni ya Watanzania. Hawa ni wana CCM ambao wanaendelea kuvalia magamba kwa nje lakini mioyoni mwao wamevalia magwanda na kila wakati wanaitika kimoyo kimoyo “Peopleeeeeeeees! Poweeeeeeeeeeer!
Katika kundi hili wamo watumishi wa umma. Hawa kwa miaka yote wamekuwa hawana magamba kwa nje lakini kwa ndani wamevalia magamba hata kama ni kwa kulazimishwa na mazingira.
Ushauri wa bure kwa CCM ni kwamba mafuriko hayajawahi kuzuiwa na kitu chochote. Acheni kujisumbua. Naona kama mmeanzisha M4K (Movement for Killing), wameuawa watu wengi sana Igunga baada ya uchaguzi mdogo wa Oktoba mwaka jana na sasa Arumeru Mashariki, pia wameanza kuuawa na wote ni viongozi na makada wa CHADEMA.
Na vitisho vinaendelea, hivi sasa vimefika kwa viongozi wetu wa wilaya na wabunge wetu kina Nassari na mwenzake aliye likizo, Lema. Mbona mnaniacha Kamanda mkuu wa mkoa mnaelekea kwa walio chini yangu tu? Njoni kwangu basi, mimi niko tayari kuingia kwenye orodha ya wafia nchi hii, kwa sababu najua baada ya kifo changu wako wengi watakaokombolewa!
Hivi hamjui damu ya Dennis Shirima, Ismail na wenzao wengi waliokufa wakati wa maandamano ya Januari 5 mwaka jana ndiyo imezidi kuleta mapinduzi Arusha mpaka kufikia hapa ilipo!? Tulieni muone damu ya Msafiri Mbwambo inavyoigeuza Arumeru Mashariki na Tanzania nzima.
Eee Mungu wajalie uhai kina Kikwete, Lowassa, Mangula, Mkapa, Msekwa, Malecela, Mkama, Nnauye, Sitta, na wenzao wote ili siku nchi hii itakapokombolewa washuhudie kwa macho yao, hata kama sijui siku hiyo watazificha wapi nyuso zao.

No comments:

Post a Comment