JUMATATU, JUNI 25, 2012 05:20
NA BENJAMIN MASESE, DAR ES SALAAM
Gazeti La MTANZANIA
ALIYEKUWA
Mlinzi wa Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ),
Maalim Seif Sharif Hamad, anadaiwa kuwa miongoni mwa wafuasi wa kikundi
cha Uamsho visiwani humo.
Taarifa zilizopatikana kutoka Mjini Zanzibar zinasema kuwa, mlinzi huyo
wa zamani wa Maalim Seif, Rashid Ally Nyange, alionekana akiwa katika
msafara wa kiongozi wa Shura ya Maimamu Zanzibar, Farid Hadi Ahmed,
wakati akitoka kuswali katika Msikiti wa Mbuyuni Unguja hivi karibuni.
Mmoja wa wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema:
“Mlinzi huyo wa Maalim Seif ni mmoja kati ya walinzi watatu wa karibu wa
kiongozi huyo wa dini, anayeongoza kikundi cha jumuiya ya Uamsho.
“Sisi wananchi tumesikitishwa sana tulipoona picha ya kiongozi wa Shura
ya Maimamu Zanzibar, Sheikh Farid katika gazeti moja la kila siku
akilindwa na aliyekuwa mlinzi wa Maalim Seif.
“Sisi kama wanachama wa CUF tunahoji sababu za mlinzi huyo wa Maalim
Seif kumlinda kiongozi huyu wa dini na aliajiriwa lini au ameagizwa na
Katibu Mkuu wetu Seif kumlinda kiongozi huyo wa dini,” alihoji mtoa
taarifa huyo.
Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki iliyopita Dar es Salaam,
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, alisema baada ya Maalim Seif
kuwa, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, waliokuwa walinzi wake wa
karibu waliachishwa kazi kwa barua rasmi.
Mtatiro alikiri kwamba, Nyange ni mmoja kati ya waliokuwa walinzi wa
karibu wa Maalim Seif na kuongeza kwamba, hivi sasa siyo mlinzi tena na
hawajui anafanya kazi gani.
“Hivi sasa Maalim Seif analindwa na walinzi wa Serikali na wale walinzi
wake wa awali, waliachishwa kazi kwa barua na hatujui walipo sasa na pia
hao walinzi hawazuiwi kuajiriwa sehemu nyingine kwa sababu wana uzoefu
wa ulinzi.
“Kwa sasa Maalim wakati wote analindwa na walinzi wa Serikali, hata
anapokuja hapa walinzi wake hutangulia na mbwa kuja kunusanusa.
“Katika hili, sijawahi kuwaona walinzi wake wa awali, pia jambo la
kusema Maalim Seif anajihusisha na kikundi cha Uamsho ni uongo na
uzushi, kwani katika hotuba zake zote alizozitoa baada ya kutokea vurugu
hizo, alikemea sana, sasa iweje ajihusishe?
“Maalim Seif hapingi Muungano uliopo sasa, hata siku moja hajawahi
kusema, lakini mara nyingi amekuwa akiunga mkono uwepo wa Serikali tatu,
yaani Serikali ya Zanzibar, Tanganyika na Serikali ya Shirikisho na
hili siyo geni, kwani hata Katiba yetu inaeleza hivyo,” alisema Mtatiro.
Nyange alipozungumza na MTANZANIA kwa simu mwishoni mwa wiki, hakutaka
kukubali wala kukataa juu ya kujihusisha na kikundi hicho.
Katika mazungumzo yake na mwandishi wetu, Nyange alisikiliza kila alichokuwa akiulizwa, kisha akasema asante na kukata simu.
Juzi, Mwanasheria wa SMZ, Othman Masoud, aliitaka jumuiya hiyo kuacha kuwapotosha wananchi kuhusu Muungano.
Pia Masoud alionya kuwa jumuiya hiyo wanachofanya ni kuwapeleka wananchi
porini, baada ya kuacha njia safi iliyonyooka ambayo ni kusubiri kutoa
maoni katika tume ya kukusanya maoni ya kurekebisha Katiba.
Awali, Waziri asiyekuwa na wizara maalumu wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Mansour Yusuf Himid, alitangaza kuvutiwa na msimamo wa jumuiya
hiyo kuhusu Muungano, huku akisisitiza kwamba lengo la jumuiya hiyo ni
kutetea maslahi ya watu wa Zanzibar katika Muungano na kuitaka Serikali
kuwaacha wananchi wawe huru.
No comments:
Post a Comment