Kambi
ya Upinzani bungeni imeitaka serikali kuwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuchunguza vifo vya
raia vilivyotokea mikononi mwa askari polisi au vyombo vya dola. Julai
mwaka jana, Pinda aliahidi kwamba serikali ingechunguza vifo hivyo kwa
kutumia sheria ya Inquest kuchunguza mauaji ya raia wakiwa mikononi mwa
vyombo vya dola.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, akitoa maoni ya
upinzani kuhusu makadirio ya Ofisi Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa
2012/13 alisema pamoja na ahadi hiyo, bado kumekuwepo na mauaji ya
kutisha na ya kikatili kwa raia wakiwa mikononi mwa polisi. Alisema
taarifa ya Haki za Binadamu na Utawala Bora zinaonyesha kwamba vifo
hivyo vimekuwa vikiongezeka kila mwaka na hakuna hatua zozote
zinazochukuliwa.
‘Ni muhimu tukatambua kuwa kila kifo cha mtu ni tofauti na cha mwingine,
na hutokea katika mazingira tofauti. Hivyo, kwa kuzingatia kilio cha
wananchi ambao Serikali ina wajibu wa kuwalinda, vifo vyote ambavyo
vimetokea kwa sababu ya matumizi ya nguvu, kikiwamo kifo cha raia
kilichotokea akiwa chini ya uangalizi wa vyombo vya dola, ni vema
serikali ikazingatia mazingira husika,” alisema.
Alisema taarifa ya haki za binadamu ya mwaka jana inaeleza kwamba
kuanzia Januari hadi Desemba 2011, takribani watu 25 wamefariki wakiwa
mikononi mwa polisi na maafisa wengine wa ulinzi na matukio mengine
yakiwaacha zaidi ya watu 50 na majeraha.
Alikumbusha kwamba ripoti hizo zinaonyesha mauaji ya raia mikononi mwa
polisi yameendelea kuongezeka ambapo watu watano walifia mikononi mwa
polisi mwaka 2008, watu 15 mwaka 2009 hadi watu 52 mwaka 2010 na katika
kipindi cha Januari hadi Mei mwaka jana, watu 9 walikuwa wameripotiwa
kuuawa katika eneo la Nyamongo, Tarime mkoani Mara.
“Kambi ya Upinzani tunatambua kuwa taarifa hizi za mauaji zinawagusa
askari Polisi pia kwa kuwa kwa mwaka uliopita katika maeneo ya Tarime,
Tabora, Shinyanga, Arusha na Rukwa polisi watano waliuawa na
wananchi…tunaamini kuwa kuacha kuchukua hatua dhidi ya polisi wachache
wanaolichafua jeshi la polisi kwa ujumla inasababisha picha mbaya ya
taifa letu kitaifa na kimataifa,” alisema Mbowe.
Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai (Chadema), alizungumzia pia unyanyasaji wa
kisiasa unaowakuta wafuasi na viongozi wa vyama vya upinzani akieleza
kwamba matukio hayo yamekuwa yakidhihirika zaidi kwenye chaguzi ndogo za
madiwani, ubunge au vijiji na vitongoji hapa.
Alitolea mfano kujeruhiwa kwa wabunge wa Chadema wakati wa uchaguzi
mdogo wa madiwani jijini Mwanza, Aprili mwaka huu (Highness Kiwia-
Ilemelela na Salvatory Machemli- Ukerewe) walikatwa mapanga wakati wa
uchaguzi mdogo wa Udiwani wa Kata ya Kirumba na wanaosadikiwa kuwa
wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema polisi wakishindwa kuzuia
tukio hilo pamoja na kuwa walifika katika eneo la tukio tena wakiwa na
silaha.
“Manyanyaso haya hayawezi kuvumiliwa tena ni lazima kama taifa tujue
kuwa nchi hii ni ya vyama vingi vya siasa na hivyo kila raia ana haki ya
kujiunga na chama chochote cha siasa bila shinikizo. Hii ni kwa sababu
bado mikutano ya kisiasa na hata mikutano ya waheshimiwa wabunge wa
upinzani inavamiwa mara kwa mara mathalani uvamizi aliofanyiwa Mbunge wa
Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa,” alisema Mbowe.
SHEREHE ZA UHURU, TAIFA
Akizungumzia
maadhimisho mbalimbali, alisema siyo lazima sherehe zote zifanyike kila
mwaka kwa kuwa zinatumia fedha nyingi bila tija huku akiitaka Serikali
iweke wazi kiasi cha fedha kilichotumika kwenye maadhimisho ya Jubilee
ya miaka 50 tangu Tanganyika ipate uhuru. Alisema gazeti moja liliripoti
kwamba katika maadhimisho hayo, serikali ilitumia Sh. bilioni 64;
taarifa ambazo hazikuwahi kukanushwa na serikali.
“Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe tamko kuhusu matumizi hayo
pamoja na mchanganuo wake ili kutekeleza dhana nzima ya uwazi na
ukweli…taarifa za gharama za sherehe hizi za Kitaifa zikawekwa
hadharani, zikiwemo gharama za mbio za mwenge ili umma wa Watanzania
waweze kuchambua na kuona kama kweli bado ni tija na kipaumbele kwa
Taifa kuendeleza sherehe hizi kwa mfumo tulio nao leo,” alisema.
Alizungumzia tatizo la chaguzi nchini na kusema kuwa kumekuwa na
ushahidi kuwa watendaji wa serikali wamekuwa wakiingilia mchakato huo
kwa faida ya chama tawala.
Alinukuu barua ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, B.B Kichinda, ya Mei
23, mwaka huu yenye Kumb. Na FA.291/300/08/25 kwenda kwa Wakurugenzi wa
Halmashauri za Wilaya na nakala zake kusambazwa kwa wakuu wote wa Wilaya
za Mkoa wa Mara, iliyoeleza "Yah: Kusimamisha uchaguzi wa serikali za
mitaa, vijiji na vitongoji katika mamlaka za serikali za mitaa"
Alisema katika barua hiyo, Kichinda aliwaelekeza watendaji hao kwamba chaguzi hizo zinasimamishwa ili kupisha uchaguzi wa CCM.
"Kwa barua hii ni dhahiri kuwa Katibu huyu amepewa maagizo kutoka ngazi
ya juu na kwa mujibu wa tangazo la Serikali Na 51 la tarehe 17 Disemba,
2010 mwenye dhamana ya kutoa maelekezo hayo ni Waziri Mkuu kwani ndio
msimamizi mkuu wa Tamisemi... barua hii ilifuatiwa na agizo la
wakurugenzi watendaji wa Halmashauri mbalimbali za Wilaya za Mkoa wa
Mara na kusimamisha chaguzi hizo," alisema.
Alimtaka Waziri Mkuu kutoa kauli ya Serikali juu ya kusimamishwa kwa chaguzi hizo ili kupisha uchaguzi wa CCM.
No comments:
Post a Comment