JUMATATU, JUNI 25, 2012 05:16
NA BENJAMIN MASESE, DAR ES SALAAM
Na Gazeti la MTANZANIA
CHAMA
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewataka viongozi wa Serikali
na Jeshi la Polisi nchini, kuwatambua wajumbe wa nyumba 10 wa chama
hicho cha upinzani, kwa kuwa nao ni viongozi halali.
Pia kimesema kuwa, kitendo cha wajumbe hao kubaguliwa, hakiwezi kukubaliwa kwa kuwa wamechaguliwa kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na wandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa
Uchaguzi CHADEMA, Msafiri Mtemelwa, alisema hivi sasa kuna mvurugano
mkubwa wa kiutawala ndani ya jamii kuhusu wajumbe wa nyumba 10.
“Sisi zamani hatukuwa na wajumbe wa nyumba 10, lakini baada ya kuona
hatuwezi kuchukua nchi bila kuwa na mizizi hadi chini, tumeweka viongozi
hao na wanatambuliwa kisheria.
“Pamoja na kwamba wanatambulika, jambo la ajabu ni kwamba, mtu akipata
shida na kuwenda kwa mjumbe wa nyumba 10 wa Chadema kisha akapeleka
barua hiyo kituo chochote cha polisi, hatapokelewa.
“Lakini mtu huyo huyo akienda kituo cha polisi na barua ya mjumbe wa
nyumba 10 wa CCM, anasikilizwa vizuri na kupewa kila aina ya msaada
anaotaka.
“Sasa tunahoji kwa nini mjumbe wa Chadema asitambuliwe na mjumbe wa CCM
atambuliwe wakati wote hao ni wawakilishi wa vyama vya siasa?
“Huu ni ubaguzi wa hali ya juu na hatuwezi kuukubali, bila shaka hii ni
mbinu ya CCM kutaka kuendelea kuwalazimisha wananchi kwamba mabalozi wa
CCM, ndio wenye uhalali wanaotambulika katika maeneo husika.
“Kwa kifupi hatuwezi kukubali hali hii, wajumbe wetu wa nyumba 10 wapo
kisheria na wanatambuliwa kama ilivyo kwa wajumbe wa CCM,” alisema
Mtemelwa.
Mtemelwa alisema kuwa, tangu Juni mosi mwaka huu, Chadema ilipoanza
kuwaweka mabalozi katika maeneo mbalimbali nchini na kufanya kazi kama
mabalozi wa CCM, baadhi ya wananchi wamekuwa wakikosa huduma pale
wanapofika katika vituo vya polisi, ofisi za mtendaji wa kata na sehemu
nyingine za Serikali, wakiwa na barua zilizotolewa na viongozi hao.
Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa viongozi wasiowatambua wajumbe wa
nyumba 10 wa Chadema, kutoendelea na tabia hiyo vinginevyo
watachukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment