WAZIRI Kivuli wa Fedha, Kabwe Zitto, amedai kuna hofu kuwa
Hazina ya serikali imekauka, na kuitaka serikali iseme ukweli wa hali
halisi ya uchumi.
Katika taarifa yake jana, Zitto ameishukia Benki Kuu ya Tanzania
akiituhumu kwa kuficha ripoti ya hali halisi ya akiba ya taifa kwa miezi
sita bila sababu za msingi na kinyume cha taratibu.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu
za Mashirika ya Umma, alisema kuwa taarifa zilizoenea mitaani ni kwamba
serikali imefilisika, na kwamba kuna tetesi kuwa Hazina ya Taifa
(Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna
hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu.
“Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipokwenda katika tovuti ya
Benki Kuu ili kuweza kuwa na habari rasmi (authoritative) nimekuta
takwimu za Novemba 2011.
“Takwimu ya mfumuko wa bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya
Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011! Na mahali pekee ambapo wananchi
wakiwamo mawaziri vivuli na wabunge wangeweza kupata ukweli wa habari
hizo ni katika tovuti ya Benki Kuu ambayo haina ripoti yoyote tangu
Desemba mwaka jana.
“Taarifa hizi zinahusu masuala yote muhimu yanayohusu uchumi wa
Jamhuri ya Muungano na uchumi wa Zanzibar, ikiwamo taarifa za mfumuko wa
bei, mapato na matumizi ya serikali, mwenendo wa biashara ya kimataifa
na deni la taifa,” alisema Zitto.
Alimtaka Gavana wa Benki Kuu Prof. Benno Ndulu kuhakikisha taarifa ya
mapitio ya uchumi wa kila mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka,
ifikapo Jumatatu Mei 14.
BoT wakanusha
Hata hivyo, Benki Kuu ya Tanzania, imekanusha taarifa za Zitto ikidai
kuwa hazina ukweli wowote, ikimtaka afanye uchunguzi wa kutosha kabla
ya kuzungumza jambo hilo linaloweza kuleta mtafaruku katika nchi.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa maofisa waandamizi
wa BoT, alisema kuwa hadi sasa kuna akiba ya kutosha kuendesha nchi kwa
miezi minne bila kuomba msaada wala kuhitaji mkopo kutoka katika taasisi
za ndani ya nchi.
Ofisa huyo aliyezungumza baada ya jitihada za kumpata Prof. Ndulu
kushindikana, alisema hata kama taarifa hizo hazipo mtandaoni
haimaanishi kuwa taifa halina kitu ama limefilisika kama inavyodaiwa.
“Hawa wanasiasa wasiseme kitu kisichokuwa na uhakika wala
hakijafanyiwa uchunguzi. Huo ni uongo, kwa sababu kama kweli angependa
kupata usahihi wa mambo haya, angeweza kuwasiliana na gavana ama hata
mimi mwenyewe, kwa sababu tumekuwa tukifanya kazi na kuwasiliana kwa
mambo mengi.
“Nimerudi juzi kutoka nje ya nchi kikazi, na huko wahisani wetu
wamekubali kutupatia msaada mkubwa ambao kama kweli tungekuwa tumefikia
kiasi hicho anachodai, hakuna taifa ambalo lingekubali kutupa msaada,”
alisema ofisa huyo.
Aliongeza kuwa kiasi kilichopo Hazina hadi sasa ni dola za Marekani
bilioni 3.6, zinazowezesha kuagiza mahitaji yote ya bidhaa kwa miezi
minne, kinyume cha madai ya Zitto.
Alidai kuwa akiba ya Watanzania iliyoko kwenye benki za hapa nchini ni dola bilioni 1.8 hadi mwanzoni mwa Mei 2012.
|
No comments:
Post a Comment